TETESI ZA SOKA
Beki Yanga amalizana na kiungo Mghana wa Simba
BEKI wa Yanga SC Gardiel Michael amemsamehe kiungo Mghana wa Simba SC, James Kotei aliyempiga ngumi katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baina ya watani hao wa jadi Jumapili Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Hiyo ni kufuatia Mghana wa Simba SC kuomba radhi kwa kitendo chake kisicho cha kiuanamichezo Septemba 30 katika mchezo uliomalizika kwa sare ya 0-0.
“Wapendwa mashabiki wa soka, ningependa kuomba radhi kwa rafiki yangu Gardiel Michael na mashabiki wote wa soka kwa kilichotokea wakati wa mechi ya wapinzani ambayo haikuwa kitendo cha uanamichezo. Nina uhakika haitatokea tena,” amesema Kotei mapema leo
Na hiyo ilifuatia baada ya jana Msemaji wa klabu Yanga, Dismass Ten kusikitishwa na kitendo cha mchezaji huyo kushindwa japo kuombwa radhi, hivyo kudai wamepeleka mashitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi dhidi ya Mghana huyo kwa kumpiga ngumi Gardiel.
“James Kotei ni mchezaji mzuri, hajawa na rekodi ya kufanya mambo ya kihuni uwanjani, hizi mechi zina mambo mengi, yawezekana alikutwa na mambo ambayo hata yeye hajui ni kitu gani kilimkumba kimsingi ilitosha yeye kuomba radhi hata kwa kutumia mitandao ya kijamii kama mchezaji muungwana” alisema Ten jana.
“Ninashukuru kaka (James Kotei), msamaha umekubaliwa, heshima mno na upendo, yaliyotokea yamepita sasa, sisi wote ni familia moja ya soka, acha tugange yajayo,” alisema.
Pamoja na tukio hilo, pia Msemaji wa Simba SC, Hajji Sunday Manara alilalamikia kitendo cha beki Andrew Vincent ‘Dante’ wa Yanga SC kumpiga kichwa Nahodha wao, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
"Hatukuwa wajinga tulipoamua kukaa kimya, tumewasaidia wale waliokwenda kushitaki TFF na Bodi ya Ligi na hili pia walipeleke. Yule karusha ngumi na huyu kapiga kichwa,”amesema Manara na kuongeza; “Tukemee vitendo vyote vya kihuni Uwanjani siyo vya Simba tu,".
Manara amesema kwamba mchezaji anaporusha kichwa kwa mwenzake kwa dhamira ovu,haijalishi kimemuathiri kwa kiasi – lakini anastahili kutolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na dhamira pekee.
“Kama ilivyokuwa kwa Kotei, mliokwenda kumshitaki, sawa ni hivi, hatuungi mkono vitendo hivi na tunavikemea, ila tusiegemee upande mmoja, si Dante wala Kotei waliofanya sahihi, adhabu ikija ije kwa wote, wakiachiwa ni wote,”amesema Manara
Post a Comment
0 Comments