Mambo yazidi kumuendea kombo kocha wa Madrid, sasa presha yaongezeka


Kufuatia kichapo cha bao 1-0 kwenye ligi kuu ya nchini Hispania 'La Liga' kutoka kwa Deportivo Alaves Jumamosi, klabu ya Real Madrid imepata pigo lingine kutokana na majeraha ya wachezaji wake muhimu wawili.

Kocha wa klabu hiyo, Julen Lopetegui amethibitisha kuwa nyota wake, Karim Benzema na Gareth Bale wamepata majeraha katika mchezo huo, huku ikiwa haifahamiki ni lini watarejea uwanjani.

Shinikizo kwa kocha huyo limezidi kuongezeka baada ya rekodi yake ya kutoshinda michezo mfululizo ya hivi karibuni kufikia hadi michezo minne hivi sasa.

Benzema alitolewa kipindi cha kwanza huku Gareth Bale akifanyiwa mabadiliko zikiwa zimebakia dakika 10 mpira kumalizika kutokana na majeraha, ambapo bao la ushindi la Alaves likifungwa na Manu Garcia katika dakika ya 90 ya mchezo.

"Karim na Bale walipata majeraha, kwahiyo tunahitaji kufanya maamuzi kufuatia mabadiliko hayo ", amesema Lopetegui.

" Huo ndio mpira, hivyo ndivyo unavyokwenda, na leo kila aina ya udhaifu umeonekana kwetu. Tuna mapumziko ya mechi za kimataifa, tunaweza kufanyia marekebisho na kurejea katika hali yetu ", ameongeza.

Real Madrid imeshindwa kufunga bao katika michezo minne mfululizo mpaka sasa, ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1985 na itaikaribisha Levante katika mchezo wa La Liga baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa.

Post a Comment

0 Comments