Uamuzi wa TFF wapingwa, Simba na Yanga zatajwa

Vilabu mbalimbali vya ligi kuu Tanzania bara vimeonesha kutoridhishwa na uamuzi wa Shirikisho la Soka nchini TFF wa kuwatumia wachezaji wake huku ratiba ya ligi kuu ikiendelea kama kawaida.
TFF ilitoa tangazo Jumanne ya wiki hii lililokanusha tetesi za kusiamamishwa kwa ratiba ya ligi kuu kupisha mchezo wa kimataifa wa kufuzu michuano ya AFCON dhidi ya Cape Verde utakaopigwa 12, Oktoba, badala yake ikatangaza kuwa wachezaji wote walioitwa katika kikosi cha Taifa Stars wataruhusiwa kucheza mechi zao za ligi na kisha kurejea kambini.
Hatua hiyo ya TFF imemuibua Afisa Habari wa Coastal Union, Hafidh Kido ambaye amesema kuwa suala hilo sio jema katika afya ya mpira kwasababu inawapa mkanganyiko wachezaji kutokana na kupata mazoezi ya sehemu mbili tofauti.
"Binafsi kama mdau wa soka nadhani hapo TFF au bodi ya ligi kuna mambo hawajakwenda sawa, walisimamisha baadhi ya michezo hapa karibuni kwasababu tu Simba na Yanga wanataka kucheza ", amesema Hafidh.
" Kwahiyo kwetu sisi au mimi kama mdau wa soka naona jambo hili halina afya katika soka kwasababu maana ya kambi ni kwamba wachezaji wakae pamoja, waelewane na kocha afundishe vizuri. Unajua kuna mchezaji mwingine anaitwa timu ya taifa kama mshambuliaji lakini kwenye klabu yake yeye ni kiungo mshambuliaji ".
" Mwingine kwenye klabu yake anacheza kama kiungo lakini kwenye timu ya taifa anacheza kama beki, sasa akiwa kwenye klabu anapewa mazoezi ya kiungo na akiwa timu ya taifa anapewa mazoezi kama beki, sasa si unamchanganya huyo mtu ", ameongeza.
Kwa upande wa Azam Fc kupitia kwa Afisa Habari wake, Jafar Idd Maganga amesema kuwa wameiomba TFF iwapatie wachezaji wake waliopo kambini na Taifa Stars  6,Oktoba badala ya 7,Oktoba ili wapate siku mbili za kufanya mazoezi pamoja kabla ya kucheza dhili ya Coastal Union 8, Oktoba.

Post a Comment

0 Comments